Monday, January 30, 2017

FAIDA NA MADHARA YA KUTUMIA DAWA YA AINA YA PENICILLIN

FAIDA NA MADHARA YA KUTUMIA DAWA YA AINA YA PENICILLIN




Penicillin ni dawa inayotumika kutibu magonjwa yanayoambukizwa na bakteria kama vile homa ya matumbo, nimonia, matatizo mfumo wa juu wa upumuaji, matatizo katika mifupa kutoa usaha na mengineyo.


Baadhi ya dawa katika kundi hili ni penicillin ni amoxillin, ampicillin, bacampicillin, carbenicillin, cloxacillin, dicloxacillin, flucloxacillin, methicillin, mezlocillin, nafcillin, oxacillin, penicillin G, pencillin V, piperacillin, pivampicillin, pivmecillin na ticarcillin.

Dawa hii haisaidii kutibu magonjwa ya baridi, mafua na mengine yanayosababishwa na virusi.
TAARIFA MUHIMU KABLA YA KUTUMIA PENICILLIN

Mgonjwa, unatakiwa kumuuliza daktari au mfamasia juu ya madhara yanayoweza kutokea pale utakapo anza kutumia dawa hii. Baadhi ya madhara haya yanachukua muda mrefu kama ambavyo nitaeleza baadae.

Baadhi ya dawa za tiba huwa zina madhara kama zitumika sambamba na dawa nyingine. Kama unatumia dawa za kupanga uzazi mweleze daktari, mfamasia au muuguzi.

Baadhi ya dawa pia zinaweza kumdhuru mtoto alie tumboni au anayenyonyeshwa kama zitatumiwa na mjamzito au anayepanga kuwa mjamzito.

Pia mweleze dakatri au mfamasia au muuguzi kama huwa unapata mzio unapotumia baadhi ya dawa za tiba kwa wakati huo au matatizo mengine ya kiafya.

Ni vyema pia kutoa taarifa kwa daktari au mfamasi au muuguzi kabla ya kutumia penicillin kama una matatizo mengine ya kiafya kama vile magonjwa ya figo, ugonjwa unaoharibu seli za chembe chembe nyeupe (mononucleosis), kutokwa na damu mwilini, na tumbo/utumbo.
MATUMIZI SAHIHI YA PENICILLIN

Tumia dawa ya penicillin kwa kunywa na maji kabla ya kula. Kunywa dawa hii kwa glasi nane za maji.

Muulize dakatari juu ya ukubwa wa glasi ya maji. Pia baadhi ya dawa katika kundi hili zinaweza wakati umekula. Muulize daktari au mfamasia au muuguzi namna bora kutumia dawa hizi.

Kama unatumia pencillin, unashauriwa kutotumia juisi ya matunda yenye tindikali  kama vile machungwa na vinywaji vingine vya jamii hii mpaka ipite saa moja mara baada ya kutumia dawa.

Ili dawa hii iweze kukusaidia unatakiwa kutumia kwa kiwango na wakati uliolekezwa kutumia. Hupaswa kuacha kutumia dawa pasipo ruhusa ya daktari hata kama unahisi kupata nafuu au kupona.

Kama utasahau kutumia penicillin, tumia pindi unapokumbuka. Kama muda uliokumbuka unakaribia ule unaofuata, acha kutumia dawa, subiri muda unaofuata ufike ndipo utumie, na kisha uendelee na utaratibu wa kawaida.

Usigawe dawa zako kwa mgonjwa mwingine au kutibu magonjwa mengine. Unatakiwa kuweka dawa mbali na watoto na hupaswi kutumia dawa zako na mtu mwingine. pia hakikisha dawa unayotumia haijaisha muda wa matumizi.

Kama itakulazimu kununua dawa, basi nunua kutoka katika duka linalotambuliwa na Serikali. Duka la dawa linalotambuliwa na serikali ni lile lilisajiliwa na Baraza la Famasi na utaitambua kwa kuangalia cheti kilichotundikwa dukani.

TAHADHARI WAKATI UNATUMIA DAWA

Kama hali yako haitaonesha kutengemaa ndani ya siku chache baada ya kutumia dawa au kama hali yako itaonekana kuzorota wasiliana na daktari mara moja.

Baadhi ya wagonjwa naotumia penicillin wanaweza kupatwa na hari ya kuharisha. Kama hali hii itaendelea muone daktari. Usitumie dawa ya kuzuia kuharisha pasipo maelekezo ya daktari.

Matumizi ya ampicillin, amoxillin au penicillin V zinaweza kuzuia utendaji kazi wa dawa za kumeza za kupanga uzazi zenye estrogen. Mimba zisizotarajiwa zinaweza kutokea.

Matumizi ya penicillin yanaweza kusabibisha vipimo vya maabara vya kiwango cha sukari kwenye mkojo kutokuwa sahihi. Kama utatakiwa kufanya kipimo cha namna hii wakati unatumia dawa hizi, mweleze daktari.
MADHARA YANAYOTARAJIWA

Ikumbukwe kuwa kila dawa ya tiba ina madhara yanayotarajiwa unapoitumia. Madhara hayo ni ya kawaida na hayapaswi kukufanya uogope kutumia dawa.

Madhara haya yako katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni yale madhara ambayo mgonjwa akiyapata anapaswa kumwona daktari mara moja. Madhara haya ni matatizo ya kupumua, homa, kuumwa viungo, kuvimba uso, vipele na upele, kuwachwa mwili na ngozi kupauka.

Hata hivyo madhara haya hutokea mara chache. madhara mengine katika kundi hili ni maumivu ya tumbo, mkojo kupungua, kuharisha na wakati mwingie kuharisha damu, msongo wa mawazo, kuchefuchefu au kutapika, koo kuwasha, homa, macho kuwa ya njano na kutokwa na damu nyingi hata kwenye jeraha dogo. Madhara haya ni ya nadra.

Hata hivyo baadhi madhara yaliyotajwa hapo juu yanaweza kuendelea kutokea muda mrefu hata baada ya kumaliza kutumia dawa. 

Imeandikwa na

Martin Malima ni

mtaalamu wa dawa kutoka  Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA).

Available link for download